TTCL

EQUITY

Saturday, January 30, 2016

UKIMYA WA EU MARUDIO YA UCHAGUZI, FUMBO KWA TANZANIA

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salum Jecha.
 
Umoja wa Ulaya (EU) umeiweka Tanzania njiapanda baada ya kutoweka wazi msimamo wake juu ya uamuzi wa kurudiwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar na iwapo watatuma waangalizi au la.
Kwa mujibu wa taratibu, Nchi za Ulaya, Afrika na Jumuiya zake, hutuma waangalizi mbalimbali kwenye uchaguzi unaofanyika katika nchi mbalimbali ili kujiridhisha na mwenendo wa uchaguzi husika.
 
Nipashe ilitaka kujua maoni ya EU baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salum Jecha, kutangaza kurudiwa uchaguzi mkuu wa Masheha, Wawakilishi na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa utafanyika Machi 20, mwaka huu.
Kadhalika, Umoja wa Mataifa, Marekani na Jumuiya ya Afrika Mashariki, zimekuwa kimya katika kueleza kama zitapeleka waangalizi katika uchaguzi huo, ambao Chama cha Wananchi (CUF), wametangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio.
 
Msemaji wa EU nchini, Susanne Mbise, alisema juzi kuwa Umoja huo hauwezi kueleza chochote kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kwa sasa na kama watapeleka waangalizi kama ulivyofanya katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana au la.
“EU haiwezi kutoa maoni yoyote kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar, pia kutuma waangalizi,” alisema katika majibu aliyotuma kwa mwandishi wa gazeti hili.
Aidha, msemaji huyo alisema kuna taarifa ya uongo inasambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza kuwa EU imetangaza nafasi za kazi ya waangalizi katika marudio ya uchaguzi huo.
 
Katika taarifa yake, EU imekanusha vikali tangazo la kutafuta waangalizi lililosambazwa kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp na facebook wanaotumia nembo ya EU, na kwamba hawaitambui taasisi hiyo na tangazo hilo la kazi.
“Pia timu ya waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU EOM) haina taarifa za taasisi hiyo na tanagzo la kazi. Haitafuti watu wa kufanya kazi ya uangalizi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa,” alifafanua.
 
Mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana, EU EOM ilitoa wito kwa ukamilishwaji wa haraka wa mchakato wa uchaguzi Zanzibar  kulingana na kanuni za uchaguzi shirikishi, za uwazi, zinazotekelezwa kwa wakati na kuaminika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwangalizi Mkuu wa EU EOM, Judith Satgentini, alisema “EU EOM iko tayari kurejea nchini kuangalia mchakato wa uchaguzi Zanzibar pindi makubaliano ya kuendelea yatakapofikiwa".
 
Mwenyekiti wa Zec, Jecha alitoa tamko la kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, baada ya kueleza kasoro tisa zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo.
Tamko hilo limezidi kuigusa jumuiya ya ndani na ya kimataifa huku wengi wakiomba serikali ya Rais Dk. John Magufuli kuingilia kati kumaliza hali hiyo.
 
Mwaka jana, Marekani ilikwishandika barua serikali ikisihi uchaguzi huo kukamilishwa kwa kufuata matakwa ya Wanzanzibari ili Tanzania iweze kuongeza vigezo vya kupatiwa msaada wa dola za marekani milioni 472.8 sawa (Sh. bilioni 993) kutoka Shirika la Maendeleo la Changamoto za Milenia (MCC), kwa ajili ya ukuzaji wa sekta ya nishati.
 
Hata hivyo, kutokana na kushindwa kufikiwa matakwa hayo, Tanzania ikikosa fedha hizo.
Kumekuwa na mvutano baina ya chama tawala (CCM) na chama kikuu cha upinzani visiwani humo (CUF). Katika mvutano huo, CUF inataka kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, ambao mgombea urais wake, Maalim Seif Sharif Hamad, alijitangaza mshindi kwa kupata kura 200,007 dhidi ya 178,363 alizopata mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein.
 
Wakati mazungumzo ya maridhiano baina ya Maalim Seif na baadhi ya viongozi wa CCM yakiendelea, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Januari 19, mwaka huu, na kutangaza kujitoa.
Mpaka anajitoa, Maalim Seif, Rais wa Zanzibar, Dk. Shein, marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Dk. Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zainzibar, Balozi Seif Ali Iddi, walikuwa wamekutana mara tisa kwa nyakati tofauti katika vikao hivyo ambavyo vilikuwa vimetawaliwa na usiri mkubwa.
 
Kutokana na sintofahamu hiyo, mataifa makubwa kama Marekani, na Denmark, yalisusia sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika  Januari 12, mwaka huu.
Katika uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, waangalizi wa nje, wakiwamo EU na UN, walitoa tamko la kuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi na kueleza ulikuwa huru na haki. Pia waangalizi wa ndani walisema ulikuwa huru na haki.
 
CHANZO NIPASHE

No comments:

Post a Comment