TTCL

EQUITY

Wednesday, December 2, 2015

Visima vya TPDC vina gesi nyingi kuliko mahitaji ya nchi

 
 Mnara ukiwaka moto baada ya gesi kufunguliwa kutoka kisimani (MB3) Mnazi Bay, hivi karibuni.

KATIKA siku za hivi karibuni, kumekuwapo mjadala katika jamii nchini juu ya uwepo wa gesi inayozalishwa kwa sasa, ambapo baadhi ya wananchi walijikuta wakiaminishwa kuwa hakuna gesi inayozalishwa kabisa na wengine wakisema gesi inayozalishwa ipo, lakini ni kidogo.
Mjadala huo ulisambaa zaidi wakati wa majaribio ya mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam, baada ya kuibuka taarifa potofu iliyosambaa mitandaoni kwamba upatikanaji wa gesi asilia ni mdogo kuliko uwezo wa mitambo ya ufuaji umeme. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limekuwa likizalisha gesi asilia ya Mnazi Bay mkoani Mtwara na Songo Songo mkoani Lindi, ambayo ni nyingi kuliko mahitaji.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio, alisema kiasi cha gesi kinachopatikana kwa sasa katika maeneo hayo ni jumla ya futi za ujazo milioni 240 za gesi asilia kwa siku. Kiasi hicho cha gesi, ni tofauti na gesi iliyogunduliwa kuanzia Mwaka 2010 katika Bahari Kuu, ambayo hadi kufikia Juni 2015, jumla ya kiasi cha gesi kilichogunduliwa huko baharini pamoja na kilichogunduliwa nchi kavu kilifikia takribani futi za ujazo trilioni 55.24.
Kwa mujibu wa Dk Mataragio, matumizi ya nchi mpaka sasa ni futi za ujazo milioni 140 za gesi asilia tu kwa siku, hivyo kuwa na ziada ya takribani futi za ujazo milioni 100 kwa siku ambazo zinapatikana Songo Songo na Mnazi Bay katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Historia ya gesi hiyo Ni vyema kufahamu kwamba utafutaji wa mafuta na gesi asilia hapa nchini, ulianza mwanzoni mwa miaka ya 1950 wakati wa Ukoloni na gesi hiyo asilia, iligunduliwa kwa mara ya kwanza kisiwani Songo Songo mwaka 1974.
Pamoja na ugunduzi huo, utafutaji uliendelea kufanywa na Kampuni ya Agip ya Italia, ambapo baadaye mwaka 1982, gesi zaidi ikagundulika Mnazi Bay, mkoani Mtwara. Hata hivyo, kampuni hiyo ya Agip ya Italia, haikuona umuhimu wa kuanza kuvuna gesi hiyo, kwa kuwa ilionekana kuwa iko kidogo na hivyo isingekuwa na tija, ikilinganishwa na gharama ambazo zingehitajika katika kuwekeza mitambo ya uvunaji wake.
Taarifa zinaonesha kuwa, Serikali haikukata tamaa hivyo ikaipatia TPDC jukumu la kuendeleza utafiti wa rasilimali hiyo kwenye maeneo yaliyoachwa na kampuni hiyo kutoka Italia. Matokeo ya shughuli za TPDC yakazaa matunda, ambapo inaelezwa kuwa ugunduzi wa gesi zaidi ulifanyika baada ya kuchimba visima vya uendelezaji huko Songo Songo na baadaye Mnazi Bay.
Kutokana na ugunduzi huo, Serikali ikaanza kujenga miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi, ambapo Oktoba 2004, matumizi ya gesi kutoka Songo Songo yakaanza kuzalisha nishati nchini na kufuatiwa na matumizi ya gesi asilia kutoka Mnazi Bay yaliyoanza mwaka 2006. Changamoto Taarifa za TPDC, zinaonesha kuwa ugunduzi wa gesi zaidi huko Songo Songo na Mnazi Bay, uliendelea hivyo miaka minne tu tangu kuanza kutumika kwa gesi kutoka maeneo hayo, miundombinu ya kuchakata na kusafirishia gesi hiyo, ikashindwa kuhimili wingi wa gesi kutokana na udogo wake.
Kutokana na changamoto hiyo, Serikali ikalazimika kujenga miundombinu mikubwa zaidi ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya kuchakata na kusafirisha gesi, ambapo kukajengwa mtambo mkubwa wa kuchakata gesi katika kijiji cha Madimba, mkoani Mtwara na bomba kubwa kutoka Mtwara na Lindi kwenda Kinyerezi Dar es Salaam, katika mitambo ya kufua umeme.
Ugunduzi zaidi, uhakika Akielezea uhakika wa gesi ya Mnazi Bay, Dk Mataragio anasema Agosti mwaka huu walishuhudia uzalishwaji wa mara ya kwanza wa gesi katika kisima cha “MB-3” huko Mnazi Bay mkoani Mtwara. Anasema ilikuwa furaha kuanza kuzalisha gesi asilia ya Mnazi Bay katika kisima hicho, ambayo itaenda kuchakatwa katika mitambo iliyoko Madimba na kisha kusafirishwa hadi Kinyerezi jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Dk Mataragio, kisima hicho kipya cha “MB-3” kina uwezo wa kuzalisha gesi asilia takribani futi za ujazo milioni 20 hadi 30 kwa siku. Dk Mataragio anasema mwezi huo huo wa Agosti kulikuwa na matarajio ya kuunganisha visima vingine kwa ajili ya kutoa gesi kutoka Mnazi Bay, ikiwemo kisima namba MX-1, MB-2, MB-4, na MB-1 ambavyo vitasababisha uzalishaji wa gesi asilia kutoka Mnazi Bay kufikia futi za ujazo milioni 130 kwa siku eneo hilo la Mnazi Bay pekee.
“Baadhi ya Watanzania walikuwa hawaamini kama tungefikia siku ambayo tungeingiza gesi kwenye bomba na kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia,” anasema Dk Mataragio. Hali ya uzalisha kwa sasa Dk Mataragio anafafanua kuwa jumla ya visima vinavyopatikana Songosongo ni vitano, ambavyo ni SS-4, SS-5, SS-9, SS-10 na SS-11 na vina uwezo wa kuzalisha jumla ya futi za ujazo milioni 150 za gesi asilia.
Pamoja na uwezo huo, lakini Dk Mataragio anasema mpaka sasa ni futi za ujazo milioni 96 tu za gesi asilia kwa siku ndio zinazozalishwa kutokana na mahitaji, huku kukiwa na ziada ya futi za ujazo milioni 54 za gesi asilia kwa siku. Anafafanua kwamba upande wa Mnazi Bay mkoani Mtwara, futi za ujazo za gesi asilia zinazozalishwa ni milioni 90 kwa siku, huku futi za ujazo milioni 43 za gesi asilia kwa siku zikiwa ziada.
Matumizi ya Mtwara Kudhihirisha udogo wa matumizi ya gesi kwa sasa, Dk Mataragio anasema; “licha ya mikoa ya Lindi na Mtwara kutumia umeme unaozalishwa kwa gesi asilia, lakini mikoa hiyo inatumia futi za ujazo milioni mbili pekee za gesi asilia kufua umeme kwa siku na kuacha ziada ya futi za ujazo milioni 8 za gesi asilia kwa siku zinazotoka katika kisima kimoja tu cha MB1, kilichopo Mnazi Bay.”
Dk Mtaragio anasema ziada inasubiri ongezeko la uhitaji wa gesi hiyo na kuongeza kuwa ziada hiyo inatarajiwa kuzalisha umeme kwa kiasi kikubwa zaidi. “Niwatoe hofu Watanzania kwa kuwahakikishia uwepo wa gesi asilia ya kutosha nchini,” anaeleza Dk Mtaragio na kuongeza kuwa gesi asilia ya ziada iliyopo Mnazi Bay na Songo Songo ikitumika yote futi za ujazo takribani milioni 100 kwa siku, zina uwezo wa kuzalisha nusu ya umeme wote unaopatika nchini kwa sasa.
Dk Mataragio anasema kwa kuwa TPDC ina dhamana ya usimamizi wa masuala ya mafuta na gesi asilia pamoja na upatikanaji wa gesi hiyo. Anasema shirika hilo litaendeleza jitihada za kuendeleza maeneo ambayo yamekwishagunduliwa kuwa na gesi asilia, ili kufikia hatua ya uzalishaji. “Novemba mwaka huu, TPDC imeendesha utafiti wa awali kwa kutumia ndege maalumu inayoainisha maeneo yanayoweza kuwa na mafuta au gesi asilia siku za usoni hususan maeneo yaliyopitiwa na Bonde la Ufa,” anasema Dk Mataragio.
Mkurugenzi huyo ameainisha maeneo hayo kuwa ni Kitalu cha Ziwa Tanganyika, Kitalu cha Eyasi Wembere na Mandawa, ambako utafiti huo unatarajiwa kukamilika Januari mwakani na mikoa itakayohusika na vitalu hivyo ni Arusha, Singida, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Lindi.

No comments:

Post a Comment