TTCL

EQUITY

Wednesday, December 2, 2015

Ujenzi wa barabara ya Mwenge-Morocco waanza



SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuamuru fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za Uhuru zikajenge barabara ya Bagamoyo kipande cha kilometa 4.3 cha Mwenge – Morocco, jijini Dar es Salaam, ujenzi huo umeanza jana.
Gazeti hili lilishuhudia tingatinga mbili mali ya kampuni ya ukandarasi ya Estim katika eneo la Mwenge, yakisafisha eneo la barabara hiyo, ikiwa ni maandalizi ya upanuzi, kama maagizo ya Rais yalivyosema.
Dk Magufuli juzi aliamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharamia sherehe za Sikukuu ya Uhuru ambazo zingefanyika Desemba 9, mwaka huu, kutumika kufanya upanuzi wa barabara hiyo ya Mwenge hadi Morocco kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Aidha, tayari fedha hizo Sh bilioni nne zimepelekwa kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, ambalo limeanza kutekelezwa mara moja kupitia mkandarasi huyo, Estim wa jijini Dar es Salaam.
Dk Magufuli alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale walipokutana Ikulu Dar es Salaam juzi, kuwa ujenzi wa barabara hiyo uanze haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika barabara hiyo.
Mmoja wa wasimamizi wa ujenzi huo kutoka kampuni ya Estim ambaye hakutaka kutaja jina lake, alipohojiwa na gazeti hili kuhusu kuanza kwa ujenzi huo na utachukua muda gani, alisema taarifa zote zipo Tanroads.
Hata hivyo, jitihada za kumpata Mfugale hazikuzaa matunda baada ya kutafutwa mara kadhaa kwa simu na kuambiwa kuwa yupo kikaoni na wasaidizi wake walisema yeye ndiye mwenye taarifa kamili.

No comments:

Post a Comment