TTCL

EQUITY

Sunday, November 10, 2013

Kabila la Waha linavyozingatia afya ya uzazi

WAHA ni miongoni mwa makabila ya kibantu yenye utamaduni wa kipekee ukiwemo wa kuzingatia afya ya uzazi salama na malezi maalumu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Kabila hilo linapatikana katika mkoa wa Kigoma na lugha yao ya asili inaitwa Kiha. 
 
 
Kabila la Waha limesheheni mila na deturi zinazoliwezesha kabila hilo kuwa na sifa za kipekee ikiwa ni pamoja na utaratibu maalumu wa kulinda afya ya mama na mtoto ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa kitabu cha Waha, Historia na Maendeleo kilichoandikwa na P. Chubwa, Waha wanathamini mtoto kuanzia siku mimba inapotungwa ambapo wazazi wa mtoto, ndugu, jamaa, ukoo na majirani na jamii nzima hutakiwa kutoa ushirikiano katika malezi ya mimba hadi mtoto atakapozaliwa. Chubwa anaeleza kuwa mila na desturi za Waha zilithamini sana ustawi wa jamii, hivyo maisha ya mtoto yajadiliwa kabla na baada ya kuzaliwa na kuendelea kutathminiwa hadi siku ya kufa kwa sababu wanaamini kuwa kuna maisha baada ya kifo.
Mafunzo kwa wanandoa Waha wana desturi ya kutoa mafunzo maalumu kwa vijana waliofunga ndoa ili kuwaandaa kuwa wazazi wazuri. Mafunzo hayo hufanyika kwa nadharia na kwa vitendo ambapo vijana waliyofunga ndoa hufundishwa miiko na mbinu za kulea mimba ili kupata watoto wenye afya njema na kuepuka vifo vinavyotokana na uzazi.
 
Kwa kuwa miaka ya nyuma wasichana wengi waliolewa katika umri mdogo wakwe zao waliwafundisha jinsi ya kutambua dalili za mimba na kuhimizwa kuwaarifu waume zao mara baada ya kuona dalili hizo. Mume akishapata taarifa, huchunguza mabadiliko ya mwili ya mkewe na anapothibitisha kuwa mkewe ni mjamzito, taarifa husambazwa kwa ndugu, jamaa marafiki na majirani ili waweze kutoa huduma kwa mama mjamzito.
Miiko wakati wa ujauzito Chubwa anasema mimba hulelewa na jamii nzima inayomzunguka mama mjamzito ambapo hata wapita njia hukuchua tahadhari na kufuatilia mwenendo wa mama mjamzito ili asikiuke miiko na kufanya mambo ambayo yanaweza kumdhuru mtoto. Mama mjamzito alipangiwa mambo ya kufanya na kutofanya katika kipindi chote cha ujauzito. Wazee walimuagiza mjamzito kula chakula cha kutosha kila anaposikia njaa ili aweze kuzaa mtoto mwenye afya nzuri.
Pia aliagizwa kufanya kazi kama kawaida, kupokea mabadiliko ya mwili na kuyakubali hasa kitendo cha tumbo kuongezeka kwa haraka, mtoto kucheza au kujigusagusa ndani ya tumbo. Mjamzito katika mila ya Kiha anakatazwa kucheka au kudharau watu wenye ulemavu ili asije kuzaa mtoto mwenye ulemavu na mwiko huu unaendelea hadi sasa kama njia mojawapo ya kuhamasisha jamii kuacha kuwanyanyapaa na kuwadharau watu wenye ulemavu.
 
Kama ilivyo kwa makabila, Waha nao walikuwa na mila potofu kuwa mwanamke akila mayai atazaa mtoto asiye na nywele hivyo ilikuwa mwiko kwa wajawazito kula mayai. Hata hivyo tafiti za kitaalamu zimebainisha kuwa mayai ni miongoni mwa vyakula vyenye virutubisho hivyo wajawazito wanashauriwa kula mayai, mboga, matunda, maini, samaki, nyama na kunde ili kuboresha afya ya mama na mtoto.
Utafiti wa sasa pia unaonesha kwamba wajawazito kukatazwa kula vitu vyenye protini nyingi yakiwemo mayai lilikuwa ni suala muhimu na la kisayansi kwa zama hizo. Hii inatokana na ukweli kwamba wakati huo hakukuwa na hospitali za kisasa na hivyo walikuwa wanaepuka mama kuzaa mtoto mkubwa ambaye inaweza kuwa shida kutoka. Uaminifu katika ndoa Wanawake walipaswa kuwa na nidhamu na uaminifu wa hali ya juu katika ndoa ili kuepuka kupata magonjwa ya zinaa ambayo huweza kusababisha madhara kwa mtoto kabla na baada ya kuzaliwa.
Kadhalika Waha wana mafunzo maalum kwa mama mjamzito kwa ajili ya kumuandaa kisaikolojia ili aweze kujifungua salama. Wazee wa kike walimsimulia mjamzito juu ya uchungu anaopata mjamzito kabla ya kujifungua. Walifundishwa kutofautisha maumivu ya kawaida na maumivu ya uchungu na kutakiwa kujikaza pale atakapopatwa na uchungu. Mwanamke wa Kiha alifundishwa mbinu za kuwa na ujasiri na kutoona aibu ili aweze kujifungua kwa urahisi.
Pia alifundishwa kusukuma mtoto kwa kuzingatia maagizo ya mkunga wa jadi. Baadhi ya mambo yamebadilika na hivi sasa wanawake wanashauriwa kufika vituo vya afya na kuzingatia ushauri wa daktari na maagizo ya mkunga wa kituo cha afya ili waweze kujifungua salama. Mafunzo kwa wanaume Pia Waha wanatoa mafunzo kwa wanaume wanaotarajia kupata mtoto. Mwanaume alifundishwa jinsi ya kutoa matunzo ya kipekee kwa mke wake katika kipindi chote cha ujauzito.
Alifundishwa mbinu mbalimbali za kupokea na kukubali mabadiliko ya mwili wa mkewe na kuendelea kumpenda kwa dhati. Pia walifundishwa jinsi ya kushinda vishawishi na tamaa za mwili wakati mke akiwa mjamzito. Pia waliaswa kutokutoka nje ya ndoa kwa kuwa kitendo hicho kinaweza kusababisha maradhi hasa magonjwa ya zinaa ambayo yanaweza kumuathiri mama na mtoto anayetarajia kuzaliwa.
Wanandoa wanaotarajia kupata mtoto walifundishwa jinsi ya kujithamini na kujiweka tayari kupokea kiumbe kipya kinachohitaji upendo wa wazazi wote wawili, malezi bora, usalama, chakula, mavazi na malazi. Wanandoa walifundishwa na kuhimizwa kuzungumzia habari za mimba kwa wanaukoo wa mwanaume kwa kuwa mtoto hurithi kwa baba yake. Mume na mke walifundishwa kutenda kwa imani kwamba ni la tunda, baraka na kiini cha ndoa, familia, ukoo na jamii yote katika eneo la Buha.
Imani ya uwepo wa Mungu Waha wanaamini kuwa Muumba wa Mbingu na dunia hupita katika nyumba za watu usiku na kukamilisha kazi ya uumbaji kwa kutumia maji. Kutokana na imani hiyo wazee waliwahimiza wanandoa kuhakikisha wanaweka maji ndani ya nyumba hasa usiku kama ishara ya kusaidiana na Muumba katika uumbaji wake. Wanandoa hao walihimizwa kukubaliana na matokeo ya muumbaji na kupokea kwa upendo mtoto yeyote atakayezaliwa ili kuepuka vitendo ya ubaguzi wa kijinsia.
Hata hivyo, wanawake wa Kiha hupendelea mtoto wa kwanza awe msichana ili aweze kumtumia kama msaidizi wake wa kazi za nyumbani. Mtoto wa kike au wa kiume? Wanawake wanaamini kuwa mtoto wa kwanza akiwa wa kike nyumba inachangamka na kuwa na baraka zaidi kwa kuwa msichana huyo atasaidia kazi za kupika, kuteka maji, kutafuta kuni na kubeba wadogo zake.
Wanaume nao hupenda mtoto wa kwanza awe mvulana kwa kuwa uzao wa kwanza ukiwa wa mtoto wa kiume huwa na uhakika wa kupata mrithi wa kuendelea na kudumisha ukoo wa baba yake. Ingawa kila mwanandoa alivutia kwake, Waha wanaona umuhimu kupata watoto wa kike na wa kiume kwa kuchanganya. Familia yenye watoto wa kike na wa kiuume huwa na furaha zaidi kwa kuwa watoto wa kike walitumika kuboresha maisha ya mtoto wa kiume ambaye alionekana kuwa na thamani kubwa zaidi.

 
Hivyo watoto wa kike katika familia walitumika kufanyakazi na wakati mwingine walilazimishwa kuolewa mapema ili mahari yao itumike kwenda kuposa mke wa mtoto wa kiume. Mtoto kukaribishwa duniani Mtoto anapozaliwa alifanyiwa mila na ibada ya kumkaribisha duniani ili aweze kuishi kwa amani na usalama. Jamii iliendelea kuendelea kumtembelea mama aliyejifungua kwa lengo la kumpa hongera na kuangalia afya na maendeleo ya mtoto.
Baada ya siku 40 mtoto alifanyiwa sherehe maarufu kwa jina la Idenga ambayo ni mahususi kwa ajili ya kumtoa mtoto nje aweze kuonekana hadharani. Sherehe hiyo inahudhuriwa na wanawake ambao hukusanyika kisha kuimba na kucheza huku wakipongeza mama mzazi. Pia sherehe hiyo hutumika kama semina isiyo rasmi ambapo wanawake huhimizana na kuhamasishana kuboresha afya ya uzazi salama.

No comments:

Post a Comment