Imeandikwa na Masamba
MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Sayansi na
Uhandisi wa Kompyuta (CoICT), Dk Richard Mgaya amefariki baada ya
kuteketea ndani ya gari lake jijini Dar es Salaam juzi.
Gari la Dk Mgaya liliteketea baada ya kugongana na lori katika eneo
la Mbezi Africana, Wilaya ya Kinondoni usiku wa kuamkia juzi na kuwaka
moto uliosababisha kifo chake.
Juzi picha mbalimbali zilisambaa katika mitandao ya kijamii
zikionesha gari aina ya Toyota Prado lililopata ajali eneo hilo la
Africana baada ya kugongana na lori, baadaye ilibainika kuwa aliyekuwa
katika gari hilo ni Dk Mgaya.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema gari la Dk Mgaya liliteketea na
hata kushindwa kujulikana dereva wa gari hilo.
Alisema baadaye ndugu wa marehemu ndio walithibitisha kuwa gari hilo
lililoteketea na dereva aliyekuwemo ni Dk Mgaya ambaye hata hivyo naye
aliteketea ndani ya gari hilo.
“Lile gari liliungua na hakuna kitu kilichopatikana, hata wakati
polisi wanafika eneo la tukio walikuta tayari dereva amekuwa majivu
kutokana na kuteketea kwa moto… labda baada ya kupima vinasaba ndio
itathibitika kama ilikuwa ni yeye,” alisema Kamanda Fuime.
Alisema hata gari hilo hawakuweza kulitambua mara moja na baada ya
kufuatilia Mamlaka ya Mapato (TRA) ilibainika kuwa mmiliki wake ni Dk
Mgaya.
Alisema “ndugu wa marehemu ndio wamesema kuwa ni ndugu yao.” Dk Mgaya
alijiunga na idara hiyo miaka kadhaa iliyopita akitokea masomoni nchini
Marekani na alikuwa ni mtaalamu wa artificial intelligence.
CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment