KWA wasiomfahamu msichana huyu,
wanamuona kama chipukizi aliyeukwaa ustaa ghafla, lakini wanaofuatilia
mambo ya sanaa na burudani, wanamfahamu kitambo. Ninamzungumzia Snura
Mushi, ambaye anatamba sana na kibao chake cha Majanga...
Ni mmoja kati ya wasanii wapambanaji, wakisaka mafanikio kwa kujaribu kila aina ya njia. Amejaribu kwa muda mrefu katika filamu, lakini hakuweza kufanikiwa ‘kuchomoka’. Kama angetambua tokea mapema kuwa angeweza kuibuka mara moja katika muziki, nadhani asingepoteza muda wake mwingi kwenye filamu.
Wimbo wake wa Majanga umeiteka familia ya muziki wa mduara, huenda kwa sasa ni mmoja kati ya wasanii wachache wanaopata nafasi ya kutakiwa sana katika majukwaa na hivyo kumfanya pia awe anapata hela za kutosha.
Katika uigizaji, alifanikiwa kucheza vizuri katika filamu kadhaa, ingawa kama ninavyosema mara zote, viwango vibovu vya sinema za Tanzania vilisaidia kumfanya asing’ae!
Wimbo wa Majanga imempandisha sana chati, kwani licha ya maneno yake yaliyopangiliwa vizuri, pia midundo yake imeongeza thamani ya kibao hicho.
Lakini kama kuna kivutio zaidi katika maonyesho ya Snura, hasa katika wimbo wake huu, basi ni yeye mwenyewe. Ni kivutio kwa sababu anacheza wimbo wake kwa namna ambayo, ni mchanganyiko wa mshangao na hamasa za kingono.
Licha ya kucheza kwa umahiri mkubwa huku akikitumia zaidi kiuno chake, hali huwa tete pale anapoyatingisha na kuyatetemesha makalio yake huku akiwa amewapa mgongo mashabiki wake ambao hulipuka kwa shangwe.
Uvaaji na uchezaji wake hauvutii machoni mwa watu wenye kuzingatia maadili ya Kitanzania, kwa maana ya tabia njema. Ni kweli anashangiliwa sana, lakini natia shaka kidogo kama kinachoshangiliwa ni muziki wake au ni namna anavyocheza.
Akili yangu inaamini anashangiliwa kwa namna anavyocheza. Na kama hivi ndivyo, basi si jambo la kujivunia hata kidogo. Uchezaji wa msanii huyu, haustahili mbele ya watoto wetu wanaoupenda muziki wake na wala haupendezi machoni mwa wanaharakati wa maadili.
Binafsi ninaamini Snura ameshauwezea aina ya muziki wake huu, ndiyo maana ameanza kupata washindani kama Shilole, ambaye naye kwa bahati mbaya, anaamini katika kukata mauno, uvaaji usiofaa na ufundi wa kuchezea viungo vyake!
Uchezaji na uvaaji wake unaonekana pia nchi nzima kupitia video yake. Ni wazazi wachache wanaoweza kufurahia kuutazama wakiwa na watoto wao.
Kuna wakati nilipata kumsikia akitangaza kusaka mtu wa kumuoa. Kwa uchezaji ule jukwaani, sidhani kama anaweza kumpata mume anayemhitaji, isipokuwa watu wengi wenye tamaa ya ngono wanaweza kujitokeza. Hakuna mume makini anayeweza kukubali mkewe acheze na kuvaa namna ile.
Labda kwa faida yake binafsi nimshauri kujitazama upya kwa sababu kubadilika ni sehemu ya maisha. Kama anafikiri uvaaji na uchezaji ule ndiyo unampatia mashabiki, mimi nakataa kwa sababu najua muziki wake umekubalika, anaweza kuvaa na kucheza kawaida na bado akaendelea kuwa juu.
Ni vyema wasanii wetu wakatambua kwamba ustaa wao unawafanya wawe mfano. Huenda zile shangwe zinazotoka kwa mashabiki siyo za kumsifu kwa uhodari wake, bali ni kumzomea kwa jinsi anavyojidhalilisha.
Na pengine ni wakati muafaka pia kwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuanza kutembelea kumbi na matamasha ili kuwabaini na kujua namna gani wanaweza kushughulika na watu wa aina hii. Hatuwezi kujenga taifa lenye maadili kama kila mtu ataachiwa kufanya anachotaka kwa sababu tu ya ustaa wao.
Kama wameweza kupiga kelele hadi sasa waigizaji wa filamu wameanza kuvaa nguo zinazokubalika, hata huku kwenye muziki wa kizazi kipya inawezekana. BASATA inao uwezo wa kuzipiga marufuku video na nyimbo zisizoendana na utamadun
No comments:
Post a Comment