SWALI kuhusu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),
Jecha Salum Jecha limeilazimisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
kuahirisha kesi ya uchochezi.
Kesi hiyo inawakabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio, baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Ilala, Salum Hamduni kukataa kujibu swali la Lissu lililotaka kujua kama Jecha ana
mamlaka ya kufuta Uchaguzi Mkuu au la.
Suali hilo lilizua mvutano mkali wa kisheria, wakati
Lissu akijitetea katika kesi ya tuhuma za kuchapisha taarifa za uchochezi yenye
kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko
yaja Zanzibar’.
Lissu alimtaka Hamduni kujibu swali hilo, kwa sababu hati
ya mashitaka inaruhusu swali hilo, hali ambayo ilisababisha mvutano mkali uliosababisha
mawakili wa pande zote kuja juu na kuona kila mmoja ana haki kwa kuvutia upande
wake.
Lissu alimwambia Hamduni, “shahidi naomba unijibu swali,
Jecha ana mamlaka ya kufuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar?”
Hamduni alikaa kimya huku Wakili wa Serikali, Paul
Kadushi akisimama kupinga swali hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
“Hakimu shahidi si mwanasheria wala si mtafsiri wa sheria
na wala si mtaalamu wa Katiba ya Zanzibar kwa hiyo napinga kujibu swali hilo,” alisema Kadushi.
Jibu la Kadushi lilimfanya Lissu apaze sauti kwa kudai
kuwa wakili wa Serikali anamlisha maneno ambayo hajayasema na pia anatakiwa
ajibu kwa sababu katika hati, mashitaka ya pili yanahusiana na swali alilouliza.
Pia Lissu alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka shahidi
amweleze kama ilikuwa ni halali yeye kushitakiwa katika kesi hiyo, kutokana na
kwamba yeye si mwandishi, mhariri, wala mmiliki wa Mawio wala mchapishaji,
lakini shahidi alimjibu kuwa inaweza ikawa halali kutegemea na mazingira.
Lissu hakukubaliana na jibu hilo na kumtaka Kamanda huyo
kumweleza ni njia gani ambayo walitumia kula njama ya kutenda kosa hilo, ambapo
majibu ya shahidi yalikuwa kwamba hajui ni njia gani walitumia wala wapi walikaa
kwa sababu kuna timu ya upelelezi ndiyo ilikuwa inashughulikia suala hilo.
Mbali na Lissu washitakiwa wengine ni Mhariri wa Mawio,
Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji
wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Kwa pamoja washitakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka
matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti
ya Mwaka 2002.
Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, mwaka jana Dar es
Salaam, washitakiwa Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha
taarifa za
uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Katika mashitaka ya pili wanadaiwa kuwa Januari 14, mwaka
jana Dar es Salaam, walichapisha habari
hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.
Mehboob anadaiwa
kuwa Januari 13, mwaka jana katika jengo la Jamana Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio
lililokuwa na taarifa za uchochezi.
Alidai mshitakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila
kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa
Msajili wa Magazeti.
Mbali na mashitaka hayo washitakiwa kwa pamoja wanadaiwa
kuwa Januari 14, mwaka jana, Dar es
Salaam, bila mamlaka waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi
Mkuu.
No comments:
Post a Comment