Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika nchini Tanzania ulitawaliwa na kasoro na vurugu zilizosababisha polisi kutumia risasi na mabomu ya machozi huku baadhi ya wapiga kura wakipigana sehemu tofauti tofauti nchini.
Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa bw. Khalist Luanda
Vurugu hizo zilitokana na uchaguzi huo kugubikwa na kasoro nyingi na hivyo kusababisha baadhi ya vituo kulazimika kuahirisha uchaguzi hadi wiki ijayo.
Vurugu hizo ziliripotiwa katika mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Kigoma, huku kasoro hizo zikitajwa kuwa baadhi ya vituo kuchanganya majina ya wagombea, kuchelewa kuanza kwa uchaguzi, kukosekana kwa vifaa vya kupigia kura na Mengineyo.
Katika vurugu zilizojitokeza Jijini Dar es Salaam Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni linawashikiliwa watu watatu kwa mahijiano zaidi kama anavyoelezeka kamanda Kamanda Camillus Wambura.
Wakati Sehemu nyingine zikitawaliwa na vurugu hizo na hatimaye kura kupigwa lakini kuna baadhi ya mikoa ikiwemo Kigoma na Ruvuma wananchi wa baadhi ya sehemu walishindwa kabisa kupiga kura kutokana na kutokukamilika kwa taratibu zingine.
Licha ya sehemu hizo imeripotiwa kuwa mamia ya wananchi wa maeneo mbalimbali mkoani Arusha wamejitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu hali iliyoashiria baadhi ya wananchi kuanza kupata uelewa na masuala ya kisiasa na kutambua haki zao.
Na katika matokeo ya awali kwa baadhi ya mikoa imeonesha kuwa sehemu kubwa ya uongozi umeangukia mikononi mwa vyama vya upinzani.
Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), nchini Tanzania Mh. Hawa Ghasia amesema serikali itawawajibisha watendaji wote wa serikali waliohusika na kuvurugika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika nchini kote hapo jana.
Akitoa ripoti ya awali ya tathmini ya uchaguzi wa serikali za mitaa Mh. Ghasia amesema kwa sasa wanafanya uchunguzi ili kubaini watendaji hao na kuongeza kuwa hata yeye akiwa waziri na msimamizi mkuu wa uchaguzi huo ikibainika alihusika kuvuruga uchaguzi huo atawajibika.
Katika tathimini hiyo ya awali ya uchaguzi wa serikali za mitaa Mh. Ghasia pia amemtaja mpiga chapa mkuu wa serikali ambae alihusika kuchapisha karatasi za kupigia kura katika baadhi ya maeneo kuchapisha karatasi hizo kimakosa na kurejeshwa kwa ajili ya kuzifanyia marekebisho lakini makosa yalionekana kujirudia tena.
No comments:
Post a Comment