TTCL

EQUITY

Thursday, June 2, 2016

TAMKO LA MH. WAZIRI JANUARY MAKAMBA KUHUSU SHUGHULI ZINAZOHITAJI KUFANYIWA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA (TAM)

TAMKO LA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) KUHUSU SHUGHULI ZINAZOTAKIWA KUFANYIWA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA (ENVIRONMENTAL IMPACT ASSESSMENT)
TAREHE 2 JUNI, 2016
Ndugu Wananchi;
Katika ulimwengu wa sasa si rahisi kutenganisha  mazingira na maendeleo. Ni wazi kuwa ufumbuzi wa matatizo ya uharibifu wa mazingira huwa mgumu kwa sababu chanzo chake kimo katika mifumo ya uendeshaji wa shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii yenye manufaa kwa uhai na ustawi wa binadamu. Shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira ndizo  hizo zinazomwezesha mwanadamu kuishi na kujiendeleza.
Hali ya mazingira inahusika sana na kuboresha “mazingira” ya vitega uchumi na kuinua kiwango cha maisha ya wananchi.  Na kwa kweli, maliasili ya mazingira ndio msingi wa maisha na maendeleo ya Watanzania.  Kwa mantiki hii, inabidi kutazama mambo mengi yanayochangia katika uharibifu wa mazingira; kutambua matatizo ya mazingira katika undani wa shughuli mbalimbali za maendeleo; kutambua sababu na kupima athari zake, na kubuni mbinu au kuchukua tahadhari za kudhibiti au kuzuia uharibifu huo bila kusimamisha wala kupunguza kasi ya shughuli za maendeleo. 
Ni kwa sababu hii serikali imepitisha sera na sheria za sekta mbalimbali zinazogusa mazingira na  imebuni programu na miradi mingi ya utekelezaji, katika kuhakikisha haya yanafanyika. 
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu, Ofisi ya Makamu wa Rais inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (SURA YA 191), pamoja na Kanuni zake. Sheria hii ndiyo Sheria mama ya masuala yote yanayohusu mazingira kwani Sheria hii inatekelezwa kwa kuzingatia sheria mbalimbali za kisekta ikizingatiwa kwamba suala la mazingira ni suala mtambuka.
Sehemu ya Sita  ya Sheria hii yenye kifungu cha 81 hadi cha 103 inaelekeza kila shughuli ya maendeleo ifanyiwe Tathimini ya Athari kwa Mazingira na inatoa ufafanuzi wa hatua za kufuata.
 Kifungu cha 81(1) kimeweka wajibu wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na kubainisha katika Jedwali la Tatu la Sheria.
Ndugu Wananchi;
Kimsingi mambo hayo yaliyotajwa  katika Jedwali la Tatu la Sheria ni ya jumla. Melezo ya kina yametolewa katika Kanuni za Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Ukaguzi za mwaka 2005. Jedwali la Kwanza la Kanuni hizi  limebainisha orodha ya  miradi ambayo inatakiwa kufanyiwa tathmini kabla ya kuanza utekelezaji wake. Orodha hii imegawanyika katika makundi mawili (2). Kundi la kwanza, yaani (A), ni la miradi ambayo  lazima ifanyiwe Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwani ni miradi ambayo inaonekana kuwa utekelezaji wake unaweza kuwa na athari kubwa kwa mazingira, hivyo utafiti wa kina unahitajika ili kubaini ukubwa wa athari na kupendekeza hatua mahsusi za kuepusha athari hizo.
Kundi la pili, yaani (B), ni miradi ambayo inaonyesha kuwa utekelezaji wake unaweza kuwa na athari kwa mazingira ingawa athari zake zinaweza kuwa ni ndogo ukilinganisha na miradi iliyotajwa katika Kundi A. Miradi hii inatakiwa kufanyiwa Tathmini ya Awali ya Mazingira (Preliminary Environmental Assessment) ili kuweza kuamua kama miradi hii inaweza kuendelea bila kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (full Environmental Impact Assessment). Hivyo kulingana na matokeo yatakayopatikana katika Tathmini hiyo ya awali miradi iliyoko katika kundi hili inaweza kuendelea bila kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira au kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira.
Shughuli au miradi inayohusika katika Kundi A, ambayo ni lazima ifanyiwe Tathmini ya Athari kwa Mazingira, ni kama ifuatavyo:-
·        Shughuli za kilimo: kilimo cha mashamba makubwa, miradi ya kilimo inayohitaji kuhamisha makazi ya wanavijiji, uanzishwaji wa matumizi ya mbegu mpya za mazao, uingizaji wa viumbe ambavyo vinasaba vyake vimefanyiwa mabadiliko ya kijenetiki n.k;
·        Usimamizi wa mifugo na maeneo ya malisho: uswagaji wa mifugo mingi, kuingizwa kwa spishi mpya au za kigeni;
·        Shughuli za misitu: ukataji wa mbao na utayarishaji, ujenzi wa barabara ndani ya misitu ya hifadhi, biashara ya mkaa, kuni na shughuli nyinginezo za uvunaji wa misitu, na kuanzisha biashara ya magogo au kubadilisha matumizi ya ardhi ya misitu kwa matumizi mengine kwenye vyanzo vya maji;
·        Shughuli za uvuvi: uvuvi wa kati na mkubwa, ufugaji mkubwa wa samaki pamoja na ufugaji wa kamba, uzalishaji na hifadhi ya minofu ya samaki viwandani;
·        Shughuli zinazohusiana na  wanyamapori: ukamataji wa wanyamapori na biashara ya wanyamapori, kuanzishwa kwa maeneo ya uwindaji yanayohusisha uhamishaji wa makazi ya vijiji,  ranchi ya wanyamapori na ufugaji na bustani na hifadhi za wanyapori;
·        Shughuli za utalii na burudani: ujenzi wa maeneo ya kutembelea au hoteli pembezoni mwa fukwe za maziwa na bahari, kingo za mito na visiwani; huduma za utalii na burudani katika maeneo yanayolindwa na maeneo yanayozunguka (mbuga za wanyama, bustani za majini, hifadhi za misitu) kwenye visiwa na maeneo yanayozunguka maji, ujenzi mkubwa kwa ajili ya michezo na burudani;
·        Shughuli za madini: uzalishaji na usambazaji wa umeme, gesi, utunzaji wa gesi asili, umeme wa maji, ujenzi wa miradi mikubwa ya nishati jadidifu na isiyo jadidifu;
·        Bidhaa za petroli: Utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, ujenzi wa mitambo ya kuzalisha mafuta na gesi, ujenzi au upanuzi wa ghala la kuhifadhia petroli, gesi, diseli, lami ndani ya maeneo ya biashara, viwanda na makazi ya watu, usafirishaji wa bidhaa za petroli;
·        Usafiri na mindombinu: ujenzi, upanuzi au ukarabati wa barabara, viwanja vya ndege, reli na eneo la kutengeneza meli au miundombinu ya bandari
·        Shughuli za chakula  na vinywaji: utengenezaji wa mafuta yatokanayo na mimea na wanyama, machinjio, usindikaji wa tumbaku;
·        Viwanda vya nguo, ngozi, mbao, kemikali;
·        Shughuli za usafishaji na utupaji taka: ujenzi wa mitambo ya uteketezaji taka, mtambo wa kuhudumia maji taka;
·        Shughuli za usambazaji maji: na
·        Shughuli za mipango ya maendeleo ya ardhi, nyumba na makazi: kuanzisha makazi mapya ya watu na wanyama, miradi mikubwa ya mijini (ujenzi wa magorofa, vituo vya magari, masoko n,k), ujazaji wa ardhi ikiwa ni pamoja na ardhi chini ya maji.
Aidha shughuli zilizotajwa katika Kundi (B), ambazo ni lazima kufanyiwa Tathmini ya Awali ya Mazingira (Preliminary Environmental Assessment) ni hizi zifutazo:-
·        Ufugaji wa samaki;
·        Ufugaji wa mifugo midogo wa mjini;
·        Ukulima wa mboga na maua;
·        Uzalishaji wa mkaa;
·        Utegaji wa ndege na biashara ya ndege pori;
·        Bustani za wanyama pori na ndege;
·        Kilimo cha mjini; na
·        Utengenezaji wa vigae.
Ndugu Wananchi;
Shughuli au miradi iliyoelezwa hapo juu imetajwa kwa ufupi kwa kuwa ni vigumu kuandika vipengele vyote vilivyotajwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 pamoja na Kanuni zake kwa kuwa ni vingi mno. Hivyo, natoa wito kwa watu wote wanaotaka kuwekeza katika shughuli yoyote kuitafuta, kuisoma na kuielewa Sheria hii pamoja na Kanuni zake ili kuweza kuitekeleza kwa ukamilifu.
Ndugu Wananchi;
Mtakumbuka tarehe 29 Mei, 2016 wakati nikitoa Tamko kuhusu  maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka huu nilieleza wazi kuwa Serikali imetoa miezi miwili, hadi ifikapo tarehe 1 Agosti 2016 kwa wale wote ambao hawana Vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira katika shughuli zao  waende Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanyiwa Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit).
Napenda kutoa wito kwa mara nyingine kwa wale wote wanaofanya shughuli zilizoorodheshwa katika Kundi A na B katika Jedwali la Tatu la Sheria ya Mazingira kuhakikisha kuwa wanatembelea Ofisi za NEMC mara moja ili kuweza kupata utaratibu kamili wa kuwezesha shughuli zao kufanyiwa Ukaguzi wa Mazingira. Niseme tu wazi kuwa baada ya muda uliotajwa hapo juu kuisha hatutakuwa na uvumilivu kwa mtu yeyote ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa, ikiwemo kuzifungia shughuli hizo, kwa wale wote watakaoshindwa kutii na kutekeleza agizo hili. Hatutakubali kisingizio cha kutoijua Sheria au kutojua mahitaji ya kufanyiwa Tathmini ya Athari ya Mazingira.
Wakati huo huo, Serikali inapanga utaratibu wa kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa Vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ili upatikanaji wa vyeti hivyo usicheleweshe uwekezaji wa kibiashara au shughuli za maendeleo.
January Makamba (MB)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira
2 Juni 2016

No comments:

Post a Comment