MAPATO ya Serikali ya Tanzania yanayotokana na shughuli za uchimbaji yameongezeka kwa asilimia 28 katika kipindi cha mwaka 2013/14, kwa mujibu wa ripoti ya sita ya asasi nayoshughulika na biashara hiyo – Tanzania Extractive Industries Transparency Initiative (TEITI) – kwa kipindi kinachoishia Juni 30, mwaka jana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo iliandaliwa na BDO East Africa na kutolewa mjini Dar es Salaam na TEIT, licha ya kushuka kwa asilimia 10 kwa idadi ya kampuni zinazohusika, mapato ya serikali kutokana na sekta ya uchimbaji yaliongezeka kutoka Sh. bilioni 956 mwaka 2013 hadi kufikia Sh. bilioni 1,221.
Ripoti hiyo inasema ongezeko hilo kubwa lifikialo Sh. bilioni 265 linatokana na ongezeko la uzalishaji wa dhahabu katika kipindi cha mwaka huo kwa asilimia 10 hali kadhalika na malipo ya kodi ya taasisi yaliyofanywa na Kampuni ya Ophir Tanzania (Block 1) ltd ya Sh. bilioni 361.
Ripoti hiyo ya TEITI inalenga kusawazisha data iliyotolewa na kampuni hizo za migodi na ile ya wizara na mashirika husika. Malengo ya jumla ya zoezi hili la usawazishi ni kuisaidia serikali itambue mchango chanya unaotolewa rasilimali za madini katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi na kuelewa uwezo wake katika kuboresha usimamizi wa rasilimali ili kujumuisha na kutekeleza kikamilifu misingi na vigezo vya TEITI.
Mwelekeo wa stakabadhi za serikali kutokana na biashara ya uchumbaji katika ripoti sita za EITI zilizochotwa kutoka katika ripoti za TEITI zinaonesha kumekuwa na ongezeko la jumla ya mapato kwa asilimia 854 tangu kuwasilishwa kwa ripoti ya kwanza mwaka 2009. Ukijumlisha kampuni zote za gesi na mafuta
Kumekuwa na ongezeko la jumla la kampuni za gesi na migodi kutoka 11 mwaka 2009 hadi kufikia kampuni 59 mwaka 2014. Hata hivyo, ripoti hiyo inabainisha kwamba kampuni zilizohakikiwa mwaka 2013 zilikuwa 65.
Kodi ya taasisi iliyolipwa serikalini ilikuwa Sh. bilioni 492.490, ikiwa ni asilimia 42.49 ya mapato yaliyokusanywa ambapo kodi ya mapato (PAYE) na SDL zilichangia Sh. bilioni 162.885 ambazo ni sawa na asilimia 14.05 ya mapato yote, kwa mujibu wa ripoti hiyo.
“Orodha ya kampuni za uchimbaji zilizoteuliwa na shirika la Multi-Stakeholder Group (MSG) kwa zoezi la usawazishi lilijumuisha kampuni 38 za uchimbaji na 21 za mafuta na gesi na kufanya jumla ya kampuni kuwa 59. Karibu kampuni zote zilizohusishwa katika zoezi hilo zimeshawasilisha taratibu zao za kuripoti, isipokuwa nne.

Shughuli za uchimbaji wa madini anuai maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Shughuli za uchimbaji wa madini anuai maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Kampuni nne ambazo zimesimaisha shughuli zao nchini Tanzania na ambazo hazipo kabisa nchini hazikuwasilisha taratibu zao. Hata hivyo, jumla ya mapato yaliyopokelewa na kutangazwa na taasisi za serikali kutoka kampuni hizo, yalikuwa Sh. bilioni 2.5, ambayo ni sawa na asilimia 0.20 ya jumla ya malipo yote yaliyofanyika serikalini.
Kampuni hizo nne ni Tanzanite One Trading Ltd., Songshan Geology Minerals Co. Ltd., Afren Gabon Ltd, na Siwandu Metal Ltd.
Ripoti hiyo inasema kumekuwa na kuhitilafiana kuhusu malipo halisi kati ya yale yaliyotajwa na kampuni za uchimbaji na yale yanayofahamika na serikali mwanzoni mwa usuluhishi ambapo tofauti ilikuwa ya asilimia 1.69 ya mapato yote yaliyotangazwa na serikali.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika hitimishoo la usuluhishi, tofauti halisi ikawa Sh. 2,428,572,571, ikiwa ni asilimia 0.20 ya jumla ya malipo yote yaliyotangazwa na serikali
Ripoti hiyo pia inasema kumekuwa na upungufu wa asilimia 10 katika ukusanyaji mapato licha ya ongezeko la uzalishaji dhahabu kwa sababu ya kuporomoka kwa bei ya dhahabu mwaka 2014. Jumla ya mapato yaliyoripotiwa na kampuni hizo yalikuwa dola za Marekeni 2,146,062,181 mwaka 2014 ikilinganishwa na dola 2,361,169,479 mwaka 2013.
Kwa mujibu wa wastani wa bei ya dhahabu iliyokokotelewa kwa msingi wa takwimu za kila mwezi, watani wa bei ya dhahabu ilipungua mwaka 2014 ikilinganishwa na mwaka 2013 kutokana na wastani wa dola 1,530.88 hadi dola 1,264.99 kwa onzi ya trei, ambapo ni upungufu wa asilimia 17.
Wakati upungufu wa mapato yatokanayo na madini unasababishwa zaidi na kushuka kwa bei ya madini hayo mwaka 2014, kulikuwa pia na upungufu wa idadi ya kampuni za migodi, kutoka kampuni 46 mwaka 2013 hadi kufikia 38 mwaka 2014 kwa sababu baadhi yao zilifunga shughuli zake nchini Tanzania.
Ophir Tanzania (Block 1) Ltd ilifanya malipo ya jumla ya Sh. 361,938,833,000.00 (30%) kwa serikali ikiwa ya kwanza katika orodha ya walipaji kumi bora wa kodi kwa mwaka 2014, ikifuatiwa na Geita Gold Mine – Sh. 195,618,242,000 (16%), Bulyahulu Gold Mining Sh. 105,602,231,000 (9%), Pan African Energy Tanzania Ltd Sh. 76,907,992 (6%), na North Mara Gold Mine Sh. 66,835,788 (5%).
Kampuni nyingine katika orodha hiyo ya kampuni bora katika ulipaji kodi kwa mwaka 2014 ni pamoja na Pangea Minerals Ltd., Songas Limited, Tanga Cement Company Ltd, Tanzania Portland Cement Ltd., Statoil Tanzania AS na Resolute Tanzania Ltd.
Tanzania ilijiunga na TEITI mnamo Februari 2009 kufuatia mapendekezo yaliyokuwa kama sehemu ya utekelezaji wa upembuzi yakinifu wa kuhakiki sekta ya madini kwa mwaka 2007.
Kundi la kazi la wadau – Multi-Stakeholder Working Group (MSG) – liliundwa kusimamia utekelezaji wa EITI nchini Tanzania na liliwajumuisha wawakilishi kutoka asasi za kijamii, kampuni za uchimbaji na serikali yenyewe.