TTCL

EQUITY

Monday, December 14, 2015

Elimu yapunguza ajali barabarani

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema ajali za barabara zimepungua hadi 7,570 kwa kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu ikilinganishwa na ajali 13,466 zilizotokea kwa kipindi kama hicho mwaka jana.
Kamanda wa kikosi hicho, Mohamed Mpinga aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akikabidhi gari kwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jackson Kapongo aliyejinyakulia gari aina ya Toyota surf lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 24 katika shindano lililochezeshwa na Kampuni ya kuuza magari ya Enhance Auto.

 
Alisema katika ajali hizo, vifo vilipungua kutoka 3,437 mwaka jana hadi kufikia vifo 3,195 mwaka huu huku majeruhi wakipungua kutoka 13,495 mwaka jana hadi 8,566 mwaka huu.
Kamanda Mpinga alisema ajali hizo zimepungua kutokana na elimu ya usalama barabarani inayoendelea kutolewa kwa wananchi ambapo kwa wastani wa ajali za kila mwezi zimepungua kutoka zaidi ya 1,000 kwa mwaka jana na chini ya 1,000 kwa mwaka huu.
Alisema mara nyingi kipindi cha kuelekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ajali nyingi zaidi hutokea na kusababisha vifo na majeruhi na kuwataka wananchi kuyatumia magari yao vizuri na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali hizo.

 
“Tatizo kubwa la ajali za barabarani ni mwendokasi, magari mabovu, ulevi na kupita gari la mbele bila tahadhari hivyo tufuate sheria za usalama barabarani ili tuepukane na ajali hizi,” alisema.
Akizungumza kampuni hiyo, Mpinga alisema imekuwa ikichezesha shindano hilo kila mwaka na kushirikisha nchi mbalimbali Afrika ambapo kwa mwaka jana mshindi alipatikana kutoka Zambia, lakini kwa mwaka huu ameshinda Mtanzania hivyo ni jambo la kujivunia.
Alisema mbali na kutoa zawadi, lakini kampuni hizo za magari zina jukumu kubwa la kutoa mchango kwa usalama barabarani kwa kutoa elimu sambamba na kuuza magari yenye viwango vinavyokubalika ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

 
“Natoa mwito kwa kampuni zingine kuwekeza katika usalama barabarani na wasifikirie tu kuuza magari bali wahakikishe magari yanakuwa salama na wanaoendesha wanakuwa salama... tuagize magari yenye viwango maana ajali nyingi pia zinasababishwa na ubovu wa magari,” alisema.
Mapema Mkurugenzi wa Enhance Auto, Aatif Farooq Butt alisema mshiriki alitakiwa kushiriki kwa kuchagua mitandao yao ya kijamii kwa wingi zaidi na lilishirikisha nchi ambazo wanafanya nao biashara ikiwemo Botswana, Burundi, Jamhuri ya Congo, Malawi, Msumbiji, Sudan Kusini, Uganda, Zambia, Zimbabwe na Tanzania.