TTCL

EQUITY

Sunday, November 15, 2015

Pazia la Spika CCM lafungwa


PAZIA la kuwania nafasi ya Spika na Naibu Spika kupitia Chama Cha Mapinduzi, limefungwa jana saa kumi jioni katika Ofisi Ndogo ya chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam, huku wanachama waliojitokeza kuwania nafasi hizo wakibakia wale wale 22 wa juzi.
Gazeti hili lilipiga kambi katika ofisi hizo tangu asubuhi mpaka kipenga cha mwisho kwa siku nzima jana, lakini hakukuwa na mgombea hata mmoja aliyeongezeka kuchukua fomu ya kuwania nafasi hizo. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatib, alikuwepo tangu asubuhi katika ofisi hizo kusubiri kama kungekuwa na nyongeza ya wagombea wa nafasi hiyo na ilipofika saa kumi kamili, alifunga ofisi na kuondoka.

Juzi akizungumza katika ofisi hizo, Khatib alisema utaratibu wa uchukuaji fomu ulitoa nafasi kwa aina mbili ya wanachama wanaowania nafasi hizo; wale ambao ni wabunge na ambao si wabunge. Kwa wanachama ambao si wabunge, walipewa nafasi ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hizo kwa siku mbili za Jumatano na Alhamisi, ili kutoa nafasi ya fomu zao kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa ajili ya uhakiki wa sifa zao.
Kwa utaratibu huo, pazia la uchukuaji fomu kwa wanachama wasio wabunge, lilifungwa Alhamisi iliyopita na wanachama ambao ni wabunge walipewa nafasi mpaka jana saa kumi, ili kutoa nafasi ya uamuzi wa vikao vya juu vya CCM. Waliochukua fomu Waliochukua fomu kuwania nafasi ya Spika ni pamoja na aliyekuwa Naibu Spika katika Bunge la 10 na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Arkson na aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi.
Wengine ni Spika mstaafu, Samuel Sitta, Mbunge mteule wa Chato, Dk Medard Kalemani, Diwani wa Goba, Dar es Salaam, Mwakalika Watson, Julius Pawatila, Agnes Makune, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Ali Mwinyi, Mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, George Nangale, Simon Rubugu, Banda Sonoko na Leonce Mulenda. Pia yumo aliyewahi kuwa Naibu Waziri, Ritha Mlaki na mhitimu wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 28, Veraikunda Urio.
Kadhalika yupo aliyekuwa mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes na aliyekuwa mmoja wa wagombea 42, waliojitokeza kuwania nafasi ya urais ndani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Dk Kalokola Muzzamil. Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Philip Marmo, Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Mbunge mteule wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko.
Naibu Spika mmoja Kati ya wanachama wote waliojitokeza wakiwemo vigogo wenye uzoefu mkubwa na wasio vigogo, ni mmoja tu Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu, aliyechukua fomu ya kuwania nafasi ya Naibu Spika.
Kwa uzoefu wake, Zungu angeweza kuongeza joto katika nafasi ya Spika, ambako baadhi ya wagombea waliojitokeza hawana sifa na uzoefu wake, lakini badala yake amekuwa mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi ya Naibu Spika.
Zungu mbali na kuwa mbunge kwa kipindi cha pili sasa, pia ana uzoefu katika uongozi wa kamati za kudumu za Bunge na wa kuongoza vikao vya Bunge katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la 10. Akizungumza na gazeti hili kuhusu hatua hiyo ya Zungu, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana, alisema mgombea huyo amewania nafasi ambayo inamfaa, kwa sababu ana uzoefu.
“Huyu amegombea nafasi anayoiweza, na amefanya vizuri kuomba, anastahili iwapo ataipata,” alisema Profesa Bana. Gazeti hili liliripoti kuwa juzi liliripoti kuwa Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alionekana kufanya kampeni kwa wabunge wenzake na alipoulizwa na gazeti hili, alisema moja kwa moja kuwa Naibu Spika anayefaa ni Zungu.
Washindani Akizungumzia mchuano kati ya wagombea wa nafasi ya Spika, Profesa Bana alisema wapo wagombea wenye uzoefu na wengine wamewania nafasi hiyo kwa kutaka majina yao yasikike, ili wajiandalie njia kwa miaka ijayo. Akifafanua zaidi, Profesa Bana alisema nafasi ya Spika ambayo imeombwa na wanachama 21, baadhi yao wameiomba tu kwa lengo la majina yao kusikika ila wapo wenye nia ya kweli ya kuitaka.
Akichambua aina ya wagombea hao, alisema yupo mmoja ambaye ameomba nafasi hiyo kwa kuwa alikuwa katika nafasi za juu katika mabunge yaliyopita na huyo akasema amefanya jambo jema. Mbali na huyo aliyeshika nafasi za juu katika mabunge yaliyopita, pia Profesa Bana alisema yupo mwingine ambaye ana uzoefu usiotia shaka na analielewa Bunge hivyo akiipata nafasi hiyo, ni sahihi pia.
Anayejisafisha Profesa Bana pia alisema kati ya wagombea hao wa nafasi ya Spika, yupo mmoja ambaye anaonekana lengo lake ni jina lake lisife, kwa kuwa hapo awali aliwahi kuhitilafiana na uamuzi muhimu wa vikao chama. Wasafisha nyota Kwa mujibu wa Profesa Bana, wagombea wengine waliowania nafasi hiyo wanajitengenezea njia mwenye miaka ijayo kwani kwenye siasa wenye nia za kuwania nafasi mbalimbali huanza maandalizi mapema.
“Mfano utaona hata Rais mstaafu Jakaya Kikwete, alianza kuonesha nia ya kuwania urais mwaka 1995, mwaka huu pia wapo walioonesha nia ila si kama waliutaka kwa sasa, ni kutengeneza njia ya miaka ijayo,” alisema Profesa Bana. Sitta bungeni Katika hatua nyingine, Sitta jana alitinga viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kusalimiana na wabunge mbalimbali.
Sitta alifika katika viwanja hivyo majira ya saa tano asubuhi, ambapo shughuli ya wabunge kujisajili kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Bunge la 11 litakaloanza Jumanne ijayo ilikuwa ikiendelea kwa siku ya pili mfululizo. Alipoonekana eneo hilo kundi la waandishi wa habari wanaoripoti habari za Bunge walimfuata kutaka kuzungumza naye na kumuuliza maswali mbalimbali.
Lakini Sitta, ambaye mara kwa mara anapofuatwa na waandishi wa habari katika mazingira kama hayo huwa mwepesi kuzungumza, aliwajibu wanahabari kwamba wampe kwanza nafasi. “Niacheni kwanza ndugu zangu nifanye kazi iliyonileta hapa,” alisema na kuelekea katika meza mbalimbali ambako kulikuwa na makundi ya wabunge wamekaa. “Naitwa Samuel Sitta, nawania uspika,” alisikika akijitambulisha katika baadhi ya meza huku akitaniana na wabunge wa siku nyingi, lakini pia akipata fursa ya kufahamiana na wabunge wapya.
Baada ya kusalimiana na baadhi ya wabunge wapya waliofika jana kujiandikisha, lakini pia kubadilishana mawazo na wabunge mbalimbali wakiwemo wale waliokuwa Bunge la 11 lililomalizika Agosti 21 mwaka huu, waandishi walimfuata tena kutaka kuzungumza naye, lakini safari hii mmoja kati ya wasaidizi wake alisema unaandaliwa utaratibu wasiwe na haraka.
Tukio hilo lilifanya baadhi ya wanahabari kuanza kuona pengine kungekuwa na ugumu jana kwa Sitta aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, kwamba hakuwa na mpango wa kuzungumza na wanahabari. Baadaye majira ya saa saba mchana, msaidizi huyo aliwaambia waandishi wa habari: “Naomba mumsubiri mzee, anaingia ofisini kidogo kisha atarudi.”
Lakini baada ya tangazo hilo, Sitta alitoka eneo la viwanja hivyo na kuondoka akiwaacha wanahabari wamepigwa na butwaa bila kuzungumza naye kwa kina. Sitta aliyehudumu pia nafasi ya Spika wa Bunge la Tisa lililokuwa likijulikana kama la kasi na viwango, ni miongoni mwa makada zaidi ya 20 wa CCM walioomba kuteuliwa na chama hicho kuwania nafasi hiyo.
Muombaji huyo wa nafasi hiyo hakuwania ubunge wa jimbo la Urambo Mashariki alilolitumikia hadi Bunge lilipovunjwa mwaka huu, ambapo ameshika nyadhifa mbalimbali za Uwaziri katika Awamu ya Pili ya Serikali na ya Awamu ya Nne, akimalizia na Wizara ya Uchukuzi. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, kuanzia juzi hadi leo ni usajili wa wabunge kwa ajili ya kushiriki mkutano huo, wakati kesho saa nne asubuhi hadi saa sita mchana itakuwa kikao kwa wabunge na pia kutembelea ukumbi wa bunge, ambapo alasiri itakuwa mikutano ya kamati za vyama.
Jumanne itakuwa ni kuanza kikao cha kwanza cha Bunge na kusomwa tangazo la Rais la kuitisha Bunge, Uchaguzi wa Spika, kiapo cha Spika, wimbo wa Taifa kupigwa na baadaye wabunge wataanza kuapishwa hadi Alhamisi asubuhi. Alhamisi jioni itakuwa kuthibitisha jina la Waziri Mkuu na pia baadaye Uchaguzi wa Naibu Spika, wakati Ijumaa alasiri Rais Dk John Magufuli atahutubia bunge na baadaye itatolewa hoja ya kuahirisha Bunge.
Massaburi ajitoa Katika hatua nyingine, habari kutoka mjini Dodoma zinasema kuwa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Massaburi amejiondoa katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili kujenga umoja na mshikamano ndani ya chama. Habari za kuaminika zilieleza jana kwamba Dk Massaburi alikuwa katika mpango wa kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ili kumweleza azma yake ya kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho kama kielelezo cha kuonyesha umoja na mshikamano ndani ya chama hicho tawala.
“Ni kweli zipo taarifa kwamba wakati Kamati Kuu inakutana leo, Dk Massaburi amefikia uamuzi wa busara wa kuondoa jina lake. Na ikumbukwe kwamba yeye si wa kwanza kwani hatua kama zake za kujiondoa zimewahi kuchukuliwa na wagombea wengine miaka ya nyuma hatua ambayo ilikisaidia sana chama kujenga mshikamano na hatimaye kushinda kwa kishindo.
“Bado hatujapokea rasmi barua yake lakini mara baada ya kuipokea tutatoa taarifa rasmi juu ya uamuzi wake huo, lakini taarifa zake tumeshazipokea ndani ya Sekretarieti ya chama hapa Dodoma,” alisema mmoja wa maofisa wa Ofisi ya CCM Makao Makuu Dodoma, ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini hadi taarifa rasmi ya chama itakapotolewa.
Hadi jana wakati wabunge wakiendelea kujiorodhesha kwenye ofisi za Bunge tofauti na wagombea wengine ambao walionekana mjini humo wakiomba kura, Dk Massaburi hakuonekana. Alipopigiwa simu kuhusu kuwepo kwa taarifa za kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho, ingawa hakutaka kueleza kwa kina suala hilo alisema alikuwa akiendelea kufanyia kazi lakini yupo tayari kuchukua uamuzi wowote ambao utaonekana kuijenga CCM na kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wake.
“Nitatoa taarifa zaidi kesho (leo) inawezekana ikawa hivyo au isiwe hivyo lakini kama mnavyojua ni kwamba kinachotakiwa ni kupatikana kwa mwanaCCM mwenye uwezo na uzoefu katika kuiendesha taasisi ya Bunge. “Naamini mimi pia uwezo wangu ni mkubwa lakini katika kuheshimu dhana ya kuzidiana na hata kuheshimu uwezo wa wengine, nipo tayari kwa lolote.
“Kwa mfano mtu kama (anamtaja mmoja wa wagombea) ameomba kugombea nafasi ya uspika kwa hiyo katika muktadha huo huo wa kuhakikisha Bunge linakuwa na kiongozi mahiri na mzoefu, nitakuwa tayari kumuunga mkono ili aweze kushinda nafasi hiyo na kuliongoza Bunge chini ya Rais Magufuli.
“Watanzania wote wana hamu ya kuona kuwa anapatikana Spika anayeweza kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema Dk Massaburi. Imeandikwa na Amir Mhando, Dodoma na Regina Kumba na Ikunda Erick, Dar.

No comments:

Post a Comment