TTCL

EQUITY

Sunday, November 15, 2015

Ndoa za Watanzania ni shida!

UTAFITI wa aina yake kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, uliohoji wanawake hasa wanandoa, umebaini taasisi hiyo muhimu katika jamii, inakabiliwa na migogoro inayochangiwa zaidi na wivu wa waume, huku wanaume wa Morogoro wakiongoza nchini kwa kuonea wivu wake zao.
Kutokana na mazingira magumu ya upatikanaji wa taarifa zake, ripoti ya utafiti huo imeeleza kuwa watafiti husika, walilazimika kuhakikisha ulinzi wa faragha kwa watoa taarifa na pale mazingira ya utoaji wa taarifa yalipokuwa yakitishia faragha hiyo, watafiti walilazimika kumuacha mtoa taarifa bila kumhoji.
Aidha watoa taarifa waliruhusiwa kuwa huru kukataa kujibu baadhi ya maswali na kabla ya kuanza kuhojiwa, watoa taarifa waliarifiwa kuwa maswali hayo ni binafsi, kwa kuwa yanatafuta majibu kuhusu masuala ya uhusiano ndani ya ndoa, huku wakihakikishiwa usiri mkubwa wa majibu yao, kwamba hakuna mtu yeyote atakayeoneshwa.
Katika hilo, watafiti walienda mbali zaidi ya unyanyasaji wa kijinsia unaotokana na vipigo, tena zaidi ya unyanyasaji wa kingono na kutafuta masuala kama kutukanwa, kuzuiwa kutembelea watu au kwenda mahali, kunyimwa mapato au vyanzo vya mapato.
Wanawake waliohojiwa na utafiti huo uliofanywa hivi karibuni wakati wa kuandaa Taarifa ya Afya ya Tanzania (DHS), walitakiwa kuelezea pia tabia za waume, au washirika wao wa kiume, za kujaribu kudhibiti sehemu ya uhuru wao, kwa kuwa zimebainika kuwa chanzo kikuu cha unyanyasaji wa kijinsia.
Maswali kwa wake Baadhi ya maswali hayo, ni pamoja na kama mume amekuwa na wivu au hasira wakati mke akiwasiliana na wanaume wengine, kama mume mara kwa mara amemtuhumu mke kwa kukosa uaminifu na kama mume amemzuia mke asikutane na marafiki zake wa kike.
Mengine ni kama mume amejaribu kuzuia mke asiwasiliane na ndugu wa upande wa mke, kama mume amekuwa akisisitiza kutaka kujua alipo mke wake wakati wote na kama mume hamuamini kabisa mke wake katika masuala ya fedha.
Matokeo ni shida Majibu ya utafiti huo uliofanyika nchi nzima, yalibaini kuna tabia inayojirudia kwa wanaume kujaribu kudhibiti sehemu ya uhuru wa wake zao, ambayo imetajwa na asilimia 66 ya wake waliohojiwa na sababu kubwa imetajwa kuwa ni wivu au hasira za waume, wakati wake zao wakizungumza na wanaume wengine.
Aidha karibu asilimia 49 ya wake hao walisema kuwa waume wao wamekuwa wakisisitiza kutaka kujua kila wanapokwenda, au walipo wakati wote, asilimia 16 wakisema waume zao hawawaamini na fedha, huku asilimia 32 wakisema kuwa waume zao wamekuwa wakiwatuhumu kwa kukosa uaminifu.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, asilimia 20 ya wanaume wametajwa kwamba wamekuwa wakizuia wake zao kukutana na marafiki zao wa kike, huku asilimia 18 ya wake wakizuiwa hata kuwasiliana na familia zao.
Matokeo zaidi yanaonesha asilimia 50 ya wanawake walioachika, waliopewa talaka, au wajane, wamesema waume waliowaacha au waliowaoa baada ya kuachika, wamekuwa na tabia hizo za kuwadhibiti.
Aidha wanawake walioolewa zaidi ya mara moja, ndio wanaotajwa kudhibitiwa zaidi na waume zao kuliko wanawake walio katika ndoa yao ya kwanza. Morogoro kwa wivu Asilimia 79 ya wanawake waliohojiwa wa Mkoa wa Morogoro, wamesema waume zao wamekuwa na wivu na mara nyingine wakikasirika kuona wao wakizungumza na wanaume wengine.
Mkoa wa pili kwa kuwa na wanaume wenye wivu kwa wake zao ni Dodoma, asilimia 77.7, Pwani (77.6%); Mara (75.9); Rukwa (75.6); Ruvuma (74.5%); Tanga (74.0%); Dar es Salaam (72.6%); Manyara (71.0%) na mkoa wa kumi ni Iringa (70.7).
Mikoa mitano ambayo wanaume hawana wivu kwa wake zao ni Pemba Kusini (38.8%); Pemba Kaskazini (42.1%); Unguja Kusini (45.8%); Mjini Magharibi (48.4) na Unguja Kaskazini (49.6%).
Vipigo wajawazito Katika utafiti huo wanawake hao waliulizwa kama wamewahi kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, unaohusisha kupigwa au kutishwa na mume wakati wa ujauzito.
Matokeo yalionesha kuwa asilimia tisa ya wanawake hao wamewahi kukabiliwa na mazingira hayo ya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa ujauzito kutoka kwa waume zao. Uchambuzi wa matokeo hayo, umebainisha kuwa wanawake waliobeba ujauzito mara nyingi, kwa maana ya kujaliwa watoto wengi, wamekabiliwa na mazingira hayo ya unyanyasaji wa kijinsia kuliko wanawake waliobeba ujauzito mara chache, kwa maana ya kujaliwa watoto wachache.
Aidha wanawake waliokosa elimu, kwa maana ya ambao hawajapata elimu ya sekondari na kuendelea na wasio na mali, wamekabiliwa na mazingira hayo ya kupigwa au kutishwa na waume zaidi, kuliko wajawazito walio na elimu ya kuanzia sekondari na kuendelea na wenye mali.
Kimkoa, Dodoma imeongoza kwa kuwa na waume waliotisha au kupiga wake zao wakati wakiwa wajawazito kwa asilimia 20 na kufuatiwa na mkoa wa Mara (19.8%). Mingine ni Kagera (17.4%); Kigoma (17.3%); Ruvuma (15.8%); Mbeya (13.3%); Iringa (9.5%); Morogoro (9.0%); Shinyanga (8.5%) na wa kumi ni Arusha kwa asilimia 8.1.
Mikoa mitano ambayo matukio ya wake wenye ujauzito kupigwa au kutishwa na waume wao ni nadra ni Pemba Kaskazini (1.2%); Unguja Kusini (2.9%); Kigoma (3.4%); Dar es Salaam (3.6%) na Lindi na Mtwara ambako kote matukio hayo yameripotiwa kwa asilimia 4.6.
Vipigo kwa wake Mbali na kupiga wajawazito, Mkoa wa Dodoma pia umetajwa kuongoza kwa waume kutisha au kupiga wake zao, ambapo asilimia 70.5 ya wake zao wameripotiwa kukabiliana na mazingira hayo, ukifuatiwa na Mkoa wa Mara tena kwa asilimia 66.4.
Mingine ni Ruvuma (50.8%); Morogoro (50.1%); Kagera (49.4%); Mbeya (48.8%); Rukwa (48.2%); Singida (46.8%); Mwanza (43.6%) na wa kumi ni Iringa ambako kumeripotiwa tabia hizo kwa asilimia 42.3.
Mikoa ambayo matukio ya waume kutisha na au kupiga wake zao ni nadra kutokea ni Pemba Kaskazini (6.3%); Pemba Kusini (7.5%); Unguja Kaskazini (8.2%); Mjini Magharibi (12.7%) na Tanga (15.7%).

No comments:

Post a Comment