TTCL

EQUITY

Sunday, November 15, 2015

Juhudi binafsi kuondoa ukeketaji

Mmoja wa washiriki katika kongamano la viongozi wa mila (Laigwanan) na wanawake mashuhuri lenye lengo la kuondoa mila potofu zinazorudisha nyuma maendeleo katika jamii za wafugaji, Laigwanan John Olekulinja kutoka kata ya Malambo wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha akitoa maoni yake kwenye kongamano hilo ilililoandaliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). (Picha na UNESCO).

JAMII ya wafugaji imetakiwa kutumia juhudi zao binafsi kubadilisha mawazo na imani ya jamii, kwamba mila na desturi hazibadiliki ili kutengeneza mfumo bora mpya unaothamini maisha ya wanawake.
 
Mwito huo umetolewa na Mtaalamu wa masuala ya vyombo vya habari vya kijamii na Mkufunzi, Rose Haji wakati akiwasilisha mada kwenye kongamano la viongozi wa mila wa kabila la Wamasai (Laigwanani) na wanawake mashuhuri yenye lengo la kushawishi uondoaji wa mila potofu zinazorudisha nyuma maendeleo katika jamii za wafugaji.

Aliwataka washiriki wa warsha kusimama kidete na kutumia elimu waliyoipata katika kushawishi jamii kubadilika na kuachana na mila za ukeketaji, ndoa za utotoni na pia unyanyasaji mwingine wa kijinsia unaoonesha ubabe wa wanaume na mfumo dume.

Aliwataka wanajamii hao kutumia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, rediojamii, vikao mbalimbali vya kata na vijiji pamoja na nyumba za ibada kuhimiza watu kubadilika na kuacha mila hizo za ukeketaji na kuozesha watoto katika umri mdogo.

Aidha Haji katika kongamano hilo lililoandaliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) amewataka wanawake kuvunja ukimya na kuacha woga na kuibua vitu vinavyowanyima haki zao za msingi.

Aliwataka wanawake kujitambua ili kutumia sheria zinazowalinda kuondokana na unyanyasaji pamoja na ukatili wa kijinsia unaoendelea katika jamii za kifugaji na kuwaomba viongozi wa mila washiriki katika kuondoa mfumo dume.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bwikizo, alisema kama watu watajitokeza na kueleza ukweli serikali itachukua hatua hasa ya kulinda wanawake na watoto kupitia mamlaka iliyokabidhiwa na Katiba ya nchi.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, KatibuTawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel Kileo, amelishukuru Shirika la UNESCO kwa kuendesha mafunzo hayo ya kutoa elimu na kujenga uwezo kwa viongozi wa mila na wanawake mashuhuri ili kuondoa mila potofu katika jamii ikiwemo ukeketaji, mimba za utotoni na ndoa za umri mdogo.

No comments:

Post a Comment